IMEBAINIKA kwamba kuna mtandao wa
askari ndani ya majeshi mbalimbali ya ulinzi nchini na hasa Jeshi la
Magereza ambao unajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
Uchunguzi wa Uwazi umebaini kwamba
tayari orodha ya majina ya askari hao yamekabidhiwa kwa Kamishna
Jenerali Mkuu wa Magereza, John Minja ili kuwashughulikia kwa mujibu wa
sheria.
Kwa mujibu wa chanzo makini kilichopo
ndani ya jeshi hilo, kilisema kwamba tayari mkakati maalum umeandaliwa
ili kuwachukulia hatua askari wanaojihusisha na mtandao huo na kuahidi
kwamba hakuna mtu hata mmoja atakayepona.
“Taa nyekundu imewaka kwani baada ya
kamishna kupata orodha hiyo aliweza kuwapangua askari wakubwa katika
Gereza la Keko jijini Dar na kuwatawanya sehemu mbalimbali ili
kuhakikisha kwamba mtandao huo unakoma na biashara hiyo inafikia tamati.
“Pia, makachero makini wamewekwa
katika kila gereza hapa nchini ili kupambana na hali hiyo na majeshi
yote yatachunguzwa,” kimesema chanzo hicho.
Mkakati huo uliandaliwa kabla ya
Aprili 7, mwaka huu ambapo saa 4 usiku makachero walimnasa askari
magereza, Brighton Octavian, akiingia kazini katika Gereza la Keko
akiwa na kete 732 za Heroin kwa madai ya kuzipeleka kwa wafungwa.
Imedaiwa kuwa askari huyo ni mmoja tu
kati ya watu wanaodaiwa kuunda mtandao huo ambao pia unawashirikisha
baadhi ya raia na vigogo wa madawa ya kulevya hapa nchini.
“Kamishna Minja amethubutu kuchukua
hatua ili kurekebisha tabia na mwenendo wa magereza yetu kwa kuwa huko
nyuma hali ilikuwa mbaya na kuonekana kama sehemu ya genge la kupitisha
madawa ya kulevya kwa ajili ya wafungwa,” kilisema chanzo hicho.
Uwazi limebaini kwamba baadhi ya
askari katika magereza mbalimbali nchini wamekuwa na maisha mazuri
kuliko makamishna wa magereza, hali ambayo inawashangaza wengi.
Inadawa kwamba askari hao wamekuwa si waaminifu kutokana na kushiriki kwao katika mtandao huo wa biashara haramu.
Baada ya Kamishna Minja kuteuliwa
kuongoza jeshi hilo, aliunda tume ya kuchunguza changamoto mbalimbali na
kugundua udhaifu mkubwa katika Gereza la Keko.
Gazeti hili lilimsaka Kamanda wa
Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini, Godfrey
Nzowa na kumuuliza hatua wanazozichukua kutokana na hali hiyo.
Mbali na kumtaja askari magereza
Brighton, pia Nzowa aliongeza kuwa wapo katika mpango maalum wa kumaliza
tatizo hilo ndani ya magereza nchini.
“Askari aliyekamatwa alikutwa na kete
732, tunajipanga kuumaliza mtandao wao kwa nguvu zote,” alisema Nzowa
na kuongeza kuwa inashangaza kuona askari nao wameingia kwenye biashara
hiyo haramu.
Alipoulizwa kuhusu majeshi mengine,
Nzowa alisema wakuu wake ambao ni wa majeshi yote hawataki kabisa kuona
biashara hiyo haramu inafanyika popote pale, hivyo yupo nao bega kwa
bega kupambana na askari atakayethubutu kuifanya.
Naye Msemaji wa Jeshi la Magereza, Mtiga Omari alisema askari Brighton ameshafukuzwa kazi.
“Tumemkabidhi kwa polisi ili
ashughulikiwe kisheria na kuhusu majina ya baadhi ya askari wengine wa
magereza wanaojihusisha na biashara hiyo naomba unipe muda nifuatilie,”
alisema Kamanda Mtiga.
Jeshi la polisi linaongozwa na IGP
Said Mwema na kanda maalum inaongozwa na DCP Suleiman Kova ambao wote
wapo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani inayoongozwa na Dk Emmanuel
Nchimbi ambaye kasi yake ya utendaji kazi tangu ateuliwe kushika wadhifa
huo na Rais Jakaya Kikwete, inasifiwa na wengi.
No comments:
Post a Comment