Mtu mmoja amekufa na wengine zaidi ya 300 hawana mahali pa kuishi katika Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kubomoa nyumba zao.
Mbali na hasara hiyo, mvua hizo iliyonyesha kwa takribani siku nne sasa,
pia zimeharibu vibaya zaidi ya ekari 60 za mazao ya chakula.
Familia hizo kwa sasa zinaishi kwa kutegemea hisani kutoka kwa wasamaria wema.
Habari
zilizopatikana jana na baadaye kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya
Hai, Novatius Makunga, zilileza kuwa tayari serikali kupitia Ofisi ya
Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa, kimetoa msaada wa chakula tani 1.5 kwa
ajili ya kuhudumia waathirika wa tukio hilo.
Aidha, aliyefariki dunia kutokana na adha hiyo ametajwa kuwa ni John Mboya (45), dereva wa pikipiki mkazi wa kijiji cha Kwatito.
Dereva huyo wa bodaboda anadaiwa alifariki dunia juzi baada ya kuzidiwa nguvu na kusombwa na maji.
“Kutokana
na hali yenyewe ilivyo,tayari tumeanza kupokea misaada ya
kijamii kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mvua hizo ambazo zimeathiri
sana wananchi wa kata ya Machame Kusini na Machame-Weruweru na maeneo
mengine ya Hai mjini.
Kaya zote zilizoathiriwa na mvua hizo hivi sasa zinahifadhiwa kwa
majirani kutokana na makazi yao kubomolewa na mvua,” alifafanua Makunga.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, tathmini ya awali ya uharibifu wa
mali za wakazi hao, inaonyesha kuwa kinahitajika kiasi cha zaidi ya Sh.
milioni 46.8 kugharimia vifaa vya ujenzi yakiwamo mabati ili wananchi
hao warejee katika makazi yao ya asili.
Makunga aliongeza kuwa msikiti wa Mudio ulioko Tarafa ya Masama uliezuliwa.
Makunga alisema kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk.
Regnald Mengi, ameahidi kutoa misaada ya kijamii kwa waathirika hao
kupitia kampuni tanzu ya vinywaji baridi ya Bonite Bottlers Limited ya
mjini Moshi.
“Bado
tunaendelea kupokea misaada na ahadi za kusaidia waathirika wa
mvua hizo na Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU)
kimeahidi kutoa magunia 10 ya mahindi, matano ya maharage na mafuta ya
chakula huku kampuni ya Usagishaji nafaka ya Mono Ban ya Arusha,
ikiahidi kutoa msaada wa tani mbili za unga wa nafaka,” alisema Makunga.
Katika hatua nyingine, serikali imesema itaendelea kutoa msaada wa
chakula kwa waathirika hao kwa mwezi mmoja hadi hapo wananchi hao
watakaporejea katika makazi yao ya asili.
Alivitaja baadhi ya vijiji vilivyoathirika zaidi na mvua hizo kuwa ni
Kwatito, Mijungwani, Shirimgungani, Mijongweni na Ngosero.Vingine ni
Kilimambogo, Kikavu Chini na Lerai.
Hata hivyo, habari zilizolifikia NIPASHE baadaye zilidai kuwa umetokea
uharibifu wa madarasa matano, ofisi ya mwalimu na nyumba tatu za walimu
wa Shule ya Sekondari Kibohehe inayomilikiwa na Baraza Kuu la Waislamu
Tanzania (Bakwata).
Baadhi
ya waathirika hao, Gerald Massawe na Ambros Kihimisho, waliiambia
NIPASHE kuwa mvua hizo zimeawaathiri kwa kiasi kikubwa kwa kuwa hivi
sasa wanalazimika kulala nje huku familia zao zikishindia mlo mmoja kwa
siku.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment