Picha maarufu kwa wiki hii(na wiki zijazo) na bila shaka inayopendeza kwa wengi na vile vile kutopendeza kwa wengine ni hiyo hapo juu inayowaonyesha Mbunge wa Mbeya Mjini, Mh.Joseph Mbilinyi aka Sugu akipeana mkono na Mkurugenzi wa Clouds Media Group,Ruge Mutahaba huku kitendo hicho kikishuhudiwa na Waziri wa Vijana,Habari,Michezo na Utamaduni,Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Singida Mashariki,Tundu Lissu jijini Dar-es-salaam hivi leo. Mkono huo au mikono hiyo ni ishara kutoka kwa wawili hao kwamba wameamua kuweka tofauti zao zilizodumu kwa takribani miaka miwili pembeni na kufungua ukurasa mpya.
Nimeanza kwa kusema picha inayondeza kwa wengi na vile vile kutopendeza kwa wengine kwa sababu ninapoandika hapa tayari gumzo kubwa lishaanza hususani katika mitandao jamii (Facebook na Twitter ikiongoza)ambapo kuna uhuru wa aina yake wa kujielezea.Kuna ambao wanahisi kusalitiwa huku wengine wakihisi kuwa na nguvu mpya na ari mpya kama ile aliyoingiaga nayo Kiongozi Mkuu wa nchi hii.
Sisi hapa BC, tumeipenda picha hiyo. Tunaamini kwamba mwisho wa siku,sisi wengine tunaombea zaidi amani na upendo.Hilo ni la msingi sana wakati huu na hata wakati ujao.Kuna umuhimu wa kufanya kazi kwa kushirikiana.Hata kama hampatani,basi kuwa na nia ya kutafuta jinsi ya kufanya kazi na kufanikisha jambo fulani.
No comments:
Post a Comment