Posted Jumanne,Mei21 2013 saa 10:15 AM
In Summary
- Yanga imemtambulisha rasmi Mrisho Ngassa aliyesaini mkataba wa miaka miwili huku ikisisitiza kuwa bado mapambano yanaendelea kusaka mastaa wa kusuka kikosi cha Afrika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Fedha ya Yanga,
Ridhiwani Kikwete baada ya kutambulishwa Ngassa aliandika kwenye ukurasa
wake wa Facebook; "Mambo yameanza ndani ya Jangwani, mtani usione wivu
natengeneza timu ya Afrika." Maneno hayo yakiwa ni kuikejeli Simba baada
ya kuwapora Ngassa.
Jopo la Yanga likiongozwa na Mwenyekiti wa usajili
pamoja na kamati ya mashindano, Abdallah Bin Kleb jana, Jumatatu
walikubaliana kuwa watafanya usajili wa aina yake ingawa hakutakuwa na
mabadiliko makubwa sana kikosini kwavile timu iliyochukua ubingwa ni
imara.
Bin Kleb ambaye alifanikisha usajili wa Mbuyu
Twite, Haruna Niyonzima na Kelvin Yondani alisisitiza kwamba mambo
yanakwenda kimyakimya na watapata wachezaji wote wanaowahitaji kwavile
kocha ameshawaambia mahitaji yake kwa Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Alipoulizwa kuhusu Shomari Kapombe ambaye mkataba
wake na Simba unamalizika Desemba, Bin Kleb alicheka na kusema wanafanya
mambo yao kimyakimya na wataweka hadharani kimoja baada ya kingine kila
kinapokuwa tayari huku akisisitiza kwamba wana malengo makubwa msimu
ujao.
Alisema hawezi kuweka hadharani silaha zake
kwavile Simba wanaweza kutibua na kwamba suala la Haruna Niyonzima
'Fabregas' kusaini mkataba mpya Yanga litakamilika wiki hii:
"Nakuhakikishia Niyonzima haendi kokote si Simba wala Azam,
wanajihangaisha tu."
Ngassa alitua Jangwani kwenye makao makuu ya Yanga
majira ya saa nne asubuhi jana Ijumaa akiambatana na Bin Kleb, Mjumbe
wa kamati ya Usajili, Seif Magari, Francis Kifukwe ambaye ni Mjumbe Bodi
ya Udhamini, Kaimu Katibu Mkuu, Lawrence Mwalusako na Mussa Katabaro
ambaye ni Mjumbe Kamati ya Utendaji.
Ngassa ambaye wiki chache zilizopita aliwaambia
viongozi wa Simba wampe fungu asaini mkataba mpya alisema jana kuwa:
"Nimerudi kwenye klabu yangu ya zamani, kweli naipenda Yanga kwa mapenzi
ya dhati na nitaitumikia kwa nguvu zote. Nilipoingia Simba watu
walikuwa na woga na mimi kutokana na tetesi kuwa nina mapenzi na Yanga
lakini kama mchezaji nafahamu majukumu yangu na nikaitumikia kwa nguvu
zote."
"Na sasa ndiyo nimerejea nyumbani rasmi.
Nawashukuru mashabiki wote. Nilienda Simba kwa mkopo nikitokea Azam FC
na sasa ni mchezaji huru nimemaliza mkataba, suala la kuwa nina mkataba
na Simba ni maneno tu, sijasaini mkataba wowote na Simba,"alifafanua
Ngassa na kusema pesa na gari aina ya Verossa alipewa na Simba ili
kumshawishi baada ya awali kukataa.
Bin Kleb alidakia kuwa: "Tumemrudisha Ngassa
nyumbani na tunamkaribisha kwa nguvu zote maana alikwenda timu nyingine
kutafuta riziki tu, nampongeza kwa kuonyesha uaminifu kwa Simba kwavile
tuliongea naye mapema kama miezi sita au mitano lakini naye alionyesha
uwezo wake uwanjani na uaminifu Simba."
"Hata mechi ya juzi alijitoa kwa kucheza kiwango
cha juu na penalti alisababisha yeye, (penalti hiyo alipiga, Mussa Mudde
raia wa Uganda akakosa) ni uaminifu," alisistiza Bin Kleb na
kuthibitisha mchezaji huyo amesaini mkataba wa miaka miwili.
Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Simba, Zakaria
Hanspope alisema: "Sisi tunaishangaa Yanga. Ngassa ni mchezaji wetu, ana
mkataba wa mwaka mmoja. Tulimchukua Azam kwa mkopo wa mwaka moja, na
tukamsaininisha mkataba mwingine wa mwaka mmoja kwa ajili ya kuitumikia
Simba."
No comments:
Post a Comment