Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imesema itasikiliza maombi ya kufanya marejeo kuhusu kuliondoa shitaka la kukaidi amri halali iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam dhidi ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda (pichani) Februari 26, mwaka huu.
Hatua hiyo imefikiwa jana mahakamani hapo baada ya Sheikh Ponda
kuwasilisha upya maombi hayo kutokana na ya awali kufutwa na mahakama
hiyo kwa kukosa mashiko ya kisheria.
Kesi hiyo iliahirishwa na Jaji Augustino Mwarija baada ya upande wa Jamhuri kuomba muda wa kujibu maombi ya mshtakiwa.
Kwa upande wake, Wakili wa utetezi, Nassoro Juma, alidai kuwa maombi ya
Jamhuri hayana msingi wa kisheria kwa sababu walipokea nakala ya maombi
hayo tangu Januari 22, mwaka huu hivyo ulikuwa na muda wa kutosha
kuandaa majibu.
Juma alisema mshtakiwa yuko mahabusu tangu Agosti, mwaka 2013 bila
sababu za msingi hivyo aliomba mahakama kutupilia mbali hoja za Jamhuri
ili mshitakiwa apate haki yake.
Jaji Mwarija aliamuru upande wa Jamhuri kuwasilisha majibu Februari 24
na upande wa Utetezi kujibu Februari 25, mwaka huu na kesi hiyo
itasikilizwa Februari 26, mwaka huu.
Katika kesi ya msingi, Sheikh Ponda anakabiliwa na mashtaka ya kukaidi
amri halali, kuharibu imani za dini, kushawishi na kutenda kosa.
No comments:
Post a Comment