Thursday, 20 February 2014

CHADEMA YAMWEKEA PINGAMIZI MGOMBEA WA CCM KALENGA IKIDAI KUWA SI RAIA WA TANZANIA



MGOMBEA Ubunge Jimbo la Kalenga kupitia CHADEMA, Grace Tendega, amemuwekea pingamizi mgombea mwenzake kupitia CCM, Godfrey Mgimwa, kwa kile kinachodaiwa kuwa si raia wa Tanzania.
 
Tendega alichukua fomu ya kumwekea pingamizi hilo juzi wakati zoezi la kusitisha fomu za wagombea ukiwa umefikia kikomo. Jana majira ya mchana mgombea huyo alirudisha fomu ya pingamizi kwa msimamizi wa uchaguzi huo, Pudensiana Kisaka.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mratibu wa kanda wa CHADEMA Nyanda za Juu Kusini, Frank Mwaisumbe, alisema mgombea alimwekea pingamizi akidai kuwa si raia wa Tanzania.
 
Mwaisumbe alisema kuwa kielelezo kingine ni mgombea huyo kuleta baadhi ya wadhamini ambao si wakazi wa Jimbo la Kalenga na si wapiga kura wa jimbo hilo.
 
"Kielelezo kingine ni tarehe ya uteuzi wa mgombea wa CCM kuwa batili, ambapo ilitajwa kuwa tarehe 16 badala ya 18,"alisema Mwaisumbe.
 
Wakati huo huo, Majira ilimtafuta msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kalenga kwa simu ya kiganjani, Pudensiana Kisaka, ambapo alikiri kuwa ni kweli mgombea amerudisha fomu ya pingamizi na kusema kuwa hawezi kutolea maelezo yoyote kwa kuwa ndio kwanza taratibu zinafanyika.
 
Jitihada za kumtafuta mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM Godfrey Mgimwa ili ajibu tuhuma hizo ziligonga mwamba kutokana na kuwa na vikao vya chama na viongozi.

No comments: