Msanii akishiriki vilivyo jukwaani
Tuzo za muziki za Kilimanjaro (Kili Music Awards), zimekuwa zikifanyika mfululizo tangu mwaka 2000. Ndizo tuzo kubwa na pekee kwa aina yake katika kuenzi na kuthamini mchango wa wasanii katika ustawi wa muziki nchini.
Mwaka huu, tuzo hizo zinazodhaminiwa na Kampuni ya
Bia Tanzania (TBL) kupitia Bia ya Kilimanjaro, zimepangwa kufanyika
Juni 8, jijini Dar es Salaam.
Tuzo hizi zinazosimamiwa na Baraza la Sanaa
Tanzania (Basata) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa muziki, kwa
kiasi kikubwa zimefanikiwa kuleta mageuzi katika fani ya muziki.
Hata hivyo, katika kipindi chote cha kufanyika
kwake, yaani kwa mwaka mara moja, changamoto nyingi na malalamiko
yamekuwa kiini kinachotia dosari ubora wa tuzo hizo.
Malalamiko yanayofanana kila mwaka kutoka kwa
wasanii na wadau wengine wa muziki dhidi ya waandaaji wa tuzo hizo,
kumewafanya baadhi kuzivisha taswira ya ubabaishaji.
Wengine wamefikia hata kuzitafsiri kama ‘mradi’ wa
wachache uliokosa tija katika ustawi wa muziki wa Tanzania, jambo
ambalo halikuwa kiini cha kuanzishwa kwake.
Mara kadhaa wasanii wamekuwa wakizisusia hata pale
majina yao yanapojumuishwa kuwa ni tuzo, wengine wakilalamika mfumo
mbovu wa kuwateua wasanii wa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wasanii wengi wanalalamika utaratibu wa uteuzi kwa
washiriki wa tuzo hizo, huku baadhi wakisema umejaa upendeleo na
wengine wakisema haujawekwa wazi kwa wasanii.
Kukosea kwa uwazi unaolezwa na wadau na wasanii
pengine ndiko kunakosababisha malalamiko kuibuka kila mwaka, jambo
ambalo linaleta mitazamo tofauti.
Ni vigumu wasanii kujua kwa nini hakuteuliwa au
kwa nini msanii fulani kateuliwa kama hakuna mfumo ulio wazi na
kutambulika kwa wasanii ambao ndiyo waelekezwa wa tuzo hizo.
Pengine ni kweli kwamba, siyo malalamiko yote
kutoka kwa wadau na wasanii wa muziki yanaweza kuwa na msingi, lakini
swali la kujiuliza kwa nini malalamiko yawe hayo hayo kila mwaka.
Tunadhani ipo sababu kwa wandaaji kuyatupia macho
malalamiko hayo ili kujenga msingi wa imani ambayo tangu mwaka 2000
imekuwa ikilalamikiwa na wasanii.
No comments:
Post a Comment